Yanga yakamilisha Wiki ya Mwananchi kwa sare na Kariobangi Sharks

Yanga SC imetoshana nguvu na Kariobangi Sharks ya Kenya kwa sare ya goli 1-1 katika mtanange wa kirafiki kuadhimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi iliyofanyika jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Taifa.
Yanga ambayo ni timu yenye mataji mengi ya TPL imetumia fursa ya Wiki ya Mwananchi kuwatambulisha wachezaji wapya ambao wamesajiliwa kwa matumizi ya msimu ujao.
Dakika zote 90 zilitawaliwa na Yanga ambapo sehemu ya kiungo ilijawa na viungo watatu Mapinduzi Balama, Papy Kabamba Tshishimbi pamoja na Mohammed Issa Banka ambao waliitawanya Kariobangi eneo la kiungo.
Baada ya kosa kosa za hapa na pale kutoka kwa mshambuliaji Juma Balinya, Sadney Ukihrob na Issa Sibomana hatimaye kikosi cha Kariobangi Sharks kilipata goli kupitia kwa Patrick Otieno kunako dakika za mwanzo za kipindi cha pili.
Ilihitaji dakika 15 baadae Yanga kusawazisha goli hilo kwa njia ya penati baada ya Sadney kumshikisha mpira mlinzi wa Sharks katika hatua za kutoa mgongeo wa mwisho, kisha Issa Sibomana akafunga goli hilo kwa penati.
Kikosi cha Yanga:- Farouk Shikalo, Mustafa Suleiman, Marcelo, Ally Mtoni Sosso, Lamine Moro, Mohammed Issa, Papy Kabamba Tshishimbi, Issa Sibomana, Juma Balinya(Mrisho Ngassa), Mapinduzi Balama na Sadney Ukihrob(Moringa).
Kiujumla ulikuwa ni mchezo wenye ushindani huku kila timu zikishambuliana kwa zamu licha ya takwimu kuibeba zaidi Yanga kwani vipindi vyote viwili kuongozwa kwa umiriki, kona na mashuti yalio lenga/kutolenga lango.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends