Yanga yalamba pointi tatu kutoka Mtibwa Sugar

Kikosi cha Yanga kimeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo Jumapili.
Ushindi huo umepatikana kupitia bao pekee lililofungwa na David Molinga mnamo dakika ya 51 kipindi cha pili akimalizia pasi sukari ya Ditram Nchimbi aliyeingia ungwe ya pili kuchukua nafasi ya Patrick Sibomana.
Yanga ambayo ilihitaji matokeo chanya katika mchezo wa leo ili kuendeleza mbio za ubingwa ambao hivi sasa bingwa mtetezi Simba ndiye kinara walijikuta wakiwa katika hofu kunwa ya kupoteza kutokana na uimara wa Mtibwa Sugar hasa eneo la kiungo.
Licha ya kemea kemea pamoja na adhabu nyingi kwa siku za karibuni kutoka TFF kuhusu makosa ya waamuzi bado changamoto hiyo imeendelea kutokea, leo katika kuaamua mipira ya kuotea na kutootea ambapo Mtibwa wamenyimwa nafasi kadhaa zilizodhaniwa na waamuzi kuwa ni mchezo wa kuotea mfano mpira wa Chanongo.
Yanga imelipiza kisasi dhidi ya Mtibwa ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa kunako Mapinduzi CUP kwa mikwaju ya penati hatua ya nusu fainali kufuatia sare ya goli 1-1.

Author: Bruce Amani