Yanga yatoa burudani kwa mashabiki, yaitwanga African Lyon 3 – 1

Yanga imeibuka mshindi wa mchezo wa kirafiki mbele ya timu ya daraja la pili African Lyon kwa kuwafunga goli 3-1 mtanange uliopigwa dimba la Azam Complex jijini Dar es Salaam leo Jumapili.

Yanga ambayo inashiriki VPL imetumia mapumziko haya rasmi ya michezo iliyo kwenye kalenda ya Fifa kucheza na Lyon kukiandaa kikosi chake kuelekea michezo ijayo hasa wa Namungo FC wa Ligi.

Magoli ya Yanga yamewekwa kimiani na Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne na Michael Sarpong kwa njia ya penati baada ya TK Master kufanyiwa madhambi katika eneo la 18, mabao yote yamefungwa kipindi cha kwanza.

Bao pekee kwa Lyon ambayo hata kwenye msimamo wa kundi lao FDL sio mzuri sana limefungwa na Mwarami Abdallah kwa faulo nje kidogo ya 18.

Mechi ijayo ya Yanga itacheza dhidi ya wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika Namungo FC Novemba 22 kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Author: Bruce Amani