Yanga yatua Mwanza kuwinda ushindi dhidi ya Alliance

343

Kikosi cha mabingwa wa kihistoria katika ligi kuu Tanzania bara Yanga kimetua salama mkoani Mwanza ambako kitavaana na Alliance FC kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe la Shirikisho maarufu kama Kombe  la TFF. Mtanange huo utakuwa Jumamosi ya Machi 30, 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kupoteza mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Lipuli ya Iringa, mchezo uliochezwa dimba la Samora.

Kuelekea mchezo wenyewe uongozi wa Yanga umesema kuwa unatambua mchezo wao dhidi ya Alliance utakuwa mgumu ila watapambana kupata matokeo chanya yatakayowapa nafasi kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

Hafidh Saleh, Mratibu wa Yanga amesema wachezaji wana morali kubwa ya kupambana na wapo tayari kwa ajili ya mchezo hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi.

“Tupo tayari kwa mapambano kwa ajili ya mchezo wetu na wachezaji wana morali kubwa ili kupata matokeo, hesabu zetu ni kuona tunashinda ili tusonge mbele.

“Alliance ni timu nzuri kwa kuwa ina vijana wengi na pia tumecheza nao michezo ya ligi hivyo tunawatambua vizuri, imani yetu ni kupata matokeo ili kusonga mbele kwa sasa tunahitaji sapoti ya mashabiki,” amesema Saleh.

Yanga wakishinda mchezo wa Jumamosi watakutana na Lipuli hatua ya nusu fainali uwanja wa Samora. Hata Alliance pia nao wakishinda watamenyana na Lipuli ambayo jana ilipenya hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo kikosi cha Yanga kitaendelea kukosa huduma ya nahodha mkuu wa timu hiyo Ibrahim Ajibu ambaye bado anasumbuliwa na mishipa ya paja kwa mujibu wa Mwinyi Zahera kocha wa Wanajangwani hao. Aidha kuna wachezaji wamerejea mazoezini kama Juma Mahadhi.

Author: Asifiwe Mbembela