Yanga yawapigisha kwata Tanzania Prisons Kombe la FA

Yanga imepata ushindi muhimu wa goli 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons mchezo wa Kombe la Shirikisho la TFF hatua ya 16 bora mtanange uliopigwa dimba la Nelson Mandela mjini Sumbawanga Rukwa.

Ushindi wa Yanga umetokana na goli la mshambuliaji wa timu hiyo Yacouba Sogne akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi Saido Ntibazonkiza ungwe ya pili.

Unakuwa ushindi wa kwanza kwa kocha Nassareddine Al Nabi kufuatia kupokea kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Azam Fc mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa wikiendi iliyopita.

Mchezo wa raundi ya kwanza ambao ulikuwa wa Ligi walipokutana Uwanja wa Nelson Mandela timu zote ziligawana pointi mojamoja kwa kufunngana bao 1-1 zama za Cedric Kaze.

Baada ya mchezo huo, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Saido Ntibanzokiza amesema kuwa kwao ni furaha kusonga mbele na ni ushindi wa timu nzima kiujumla.

“Tumepata ushindi ninafurahi naamini hii ni furaha ya wachezaji kiujumla pamoja na benchi la ufundi,” amesema.

Kwa matokeo hayo, Yanga imetinga robo fainali na kuungana na Mwadui Fc, Rhino Rangers, Azam na Biashara.

Mechi nyingine zitakazopigwa Jumamosi, Simba Vs Kagera Sugar, Dodoma Jiji Vs KMC, Jumapili itakuwa mechi moja JKT Tanzania dhidi ya Namungo.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares