Zarika akwepa makonde ya Phiri na kuhifadhi taji lake

Kabla ya kupanda ulingoni, swali ambalo kila mmoja alijiuliza ni je, ataitumia fursa ya pili kumnyamazisha bingwa wa taji la WBC Super bantamweight kwa upande wa wanawake? baada ya pigano, jibu likawa ni hapana kwa sababu Mkenya Fatuma “Iron Fist” Zarika ameibuka mshindi baada ya kuzikwepa ngumi za mpinzani wake Mzambia Catherine Phiri na kuhifadhi taji lake kupitia ushindi kwa pointi. Majaji wote watatu walimpa Zarika ushindi kwa kupata pointi nyingi.

Phiri alimkabili Zarika toka mwanzo hadi mwisho

Katika pigano ambalo lilikuwa marudio ya lile la miaka miwili iliyopita, Zarika alikabiliwa vikali mwanzo hadi mwisho katika ukumbi uliofurika wa Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta – KICC jijini Nairobi.

Majaji Michael Neequaye, Fillemon Mweya na Irene Semakula walimpa ushindi kwa pointi 98-92 99-91 97-93 na kuzusha shangwe, mbwembwe na vifijo miongoni mwa mashabiki wa nyumbani waliofika kumshangilia bondia wao.

Phiri alitaka kulipiza kisasi kichapo alichopata cha 3 – 0 kupitia uamuzi wa majaji mnamo Desemba 2, 2017 kwa kumvamia Zarika lakini wakati pigano likiendelea, raundi moja baada ya nyingine, ilibainika wazi kuwa haingekuwa rahisi kwa Mzambia huyo kutimiza operesheni yake. Zarika alimzidi nguvu katika raundi ya tatu, tano na nane, wakati naye Phiri akimpiku katika raundi ya pili, nne, tano na sita.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends