Zimamoto ya Zanzibar yaizima Kaiser Chiefs

367

Je historia ipo ili ivunjwe? Kama jibu ni ndio basi itakuwa sawa na kile kilichotokea katika uwanja Amani Zanzibar ambapo timu isiyofahamika na wengi, timu yenye idadi ndogo ya mashabiki na wanachama, timu isiyo na bajeti endelevu, timu inayotokea sehemu ambayo ligi yake huendeshwa kwa mizengwe na changamoto nyingi, Zimamoto imeishangaza klabu inayotokea katika ligi yenye wadhamini wengi zaidi barani Afrika Kaiser Chiefs ya nchini Afrika Kusini kwa goli 2-1 ukiwa ni mchezo wa pili baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa Zimamoto kulala kwa goli 4-0.

Unaweza ukajiuliza kwa nini inasifiwa Zimamoto wakati imepoteza nafasi ya kuendelea na mashindano, ukweli ni kwamba Zimamoto imekuwa na matatizo mengi yenyewe kama timu mbali na changamoto za hapa na pale za ligi ya Zanzibar.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika bondeni, Zimamoto ilipoteza jumla ya goli 4-0 ilihitaji kushinda zaidi ya goli tano ingawa haikuwa hivyo, kitendo tu cha kufunga hata goli moja basi imekuwa heshima kubwa kwa kisiwa cha Zanzibar kwani ligi hiyo ipo katika marekebisho kwa lengo la kufanya kandanda lao kuwa shindani kama ligi nyingine za kandanda.

Katika mchezo wa Jumanne Desemba 4 uliofanyika katika dimba la Amani, magoli ya Zimamoto yalifungwa na Yusiffu Mtuba kunako dakika ya 23 na 75 huku goli la kufutia machozi likifungwa na Lebagang Manyama dakika ya 66.

Pamoja na ukweli kuwa Kaizer Chiefs haina muendelezo mzuri katika ligi ya Afrika Kusini ambako inashikiria nafasi ya 7 kwa alama 28 baada ya michezo 14 bado Zimamoto hawana budi kushangilia kwani ni ishara njema kwa soka la Zanzibar na Afrika Mashariki ambalo mara nyingi limekuwa kichwa cha mwenda wazimu huku soka likitawaliwa na vilabu vya kaskazini na magharibi mwa Afrika.

Haikuwa rahisi kwa Zimamoto kupata matokeo hayo yanayoweza kuwa tumaini jipya la kufanya vizuri kwenye mashindano yanayofuata kama kombe la Mapinduzi.

Mda mwingine hauhitaji kuwa na vitu vya thamani sana ndio ujithamini bali vile ulivyo, utakavyoonekana na ukijithamini kwanza wewe utaonekana wathamani zaidi.

Author: Bruce Amani