Kipchoge aweka rekodi mpya ya marathon duniani

Mkenya Eliud Kipchoge amedhihirisha kuwa yeye ndiye mwanariadha bora zaidi wa mbio za marathon ulimwenguni, baada ya kushinda taji lake la tatu la mbio za Berlin Marathon na kuweka rekodi mpya ya 2:01:40.

Kipchoge alikimbia katik nafasi ya mbele kuanzia hatua za mwanzo na kufikia mita 17 za mwisho, alikuwa peke yake kabisa, kabla ya kuivunja rekodi ya dunia kwa sekunde 76.

Sasa yeye ni mtu wa kwanza kuwahi kukimbia chini ya 2:02:00, rekodi ambayo itachukua muda mrefu kuuvunja. Rekodi ya awali iliwekwa na Mkenya Denis Kimetto katika Berlin marathon 2014.

“Nilikuwa nimejiandaa sana kwa ajili ya kuja Berlin. Niliamini katika mfumo wangu wa mazoezi, niliwaamini wakufunzi wangu” Alisema Kipchoge baada ya kuvunja rekodi. Aliongeza kuwa yeye hujiamini na hukimbia kivyake bila kuwaangalia wapinzani wake.

Mkenya Amos Kipruto alimaliza wa pili katika muda wa 2:06:22, huku Wilson Kipsang aliyewahi kuweka rekodi ya dunia akimaliza wa tatu katika muda wa 2:06:47.

Kipchoge sasa ameshinda mbio 10 za marathon kati ya 11 ambazo ameshiriki.

Author: Bruce Amani