Kipchoge, Dalilah wanariadha bora wa mwaka duniani

Eliud Kipchoge na Dalilah Muhammad wametangazwa kuwa washindi wa Tuzo ya Wanariadha bora wa mwaka duniani kwa wanaume na wanawake

Mkenya Kipchoge, mwenye umri wa miaka 35, alishinda mbio za London Marathon kwa mara ya nne mwezi Aprili kabla ya kuwa mwanariadha wa kwanza duniani kukimbia mbio za marathon chini ya saa mbili.

Muhammad, mwenye umri wa miaka 29, alishinda dhababu katika mashindano ya ubingwa wa dunia katika mbio za mita 400 kuruka viunzi mjini Doha baada ya kuvunja mara mbili rekodi ya dunia mwaka huu.

Mmarekani huyo, ambaye alishinda taji la Olimpiki mjini Rio 2016 alisema: “Umekuwa mwaka mzuri sana. Umekuwa mwaka mgumu lakini nashukuru. Sikuwahi kudhania ningeumaliza mwaka namna hii.”

Kipchoge, ambaye alishinda tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka kwa mwaka wa pili mfuulizo amesema: “Natumai ninaihimiza jamii ya mwanadamu. Nina furaha sana kwa kuweka historia. Natumai ilikuwa motisha kubwa kwa kizazi kijacho.”

Author: Bruce Amani