Kocha Koeman atajwa kuchukua mikoba ya Setien Barcelona

Klabu ya Barcelona inatajwa kumuajiri kocha Ronald Koeman kuwa kocha wao mpya baada ya kumtimua kocha Quique Setien kufuatia matokeo mabaya

Kwa mjibu wa mwandishi wa habari mkongwe Guillem Balague ni kuwa kocha Quique Setien atatimuliwa rasmi Jumatatu na kupewa kazi hiyo aliyekuwa kocha wa Uholanzi Ronald Koeman.

Barca ambayo ilipewa kichapo cha aibu siku ya Ijumaa cha goli 8-2 dhidi ya Bayern Munich robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imeamua kumtimua kocha huyo baada ya kuwa na wakati mbaya ndani ya Wanacatalunya hao.

Setien, 61, aliajiriwa kama mbadala wa Ernesto Valverde mwezi Januari mwaka huu. Balague amesema licha ya kocha wa zamani wa Tottenham Mauricio Pochettino kuhusishwa kujiunga na miamba hiyo lakini inaonekana chaguo rahisi atakuwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo Koeman.

“Bodi itakaa kesho (Jumatatu) na kocha Setien kwa ajili ya kumfuta kazi, lazima wapate kocha mpya kwani wiki mbili zijazo wanaanza maandalizi ya msimu ujao, ambapo jina la Koeman ndio lililotawala”

Kocha huyo wa zamani wa Everton na Southampton Koeman, 57, alitajwa kuwa kocha wa Uholanzi mwaka 2018 ambapo mwezi wa tano alipata shida kidogo ya kiafya lakini sasa amerejea katika afya yake.

Hata hivyo, Koeman anaweza asikaae muda mrefu ndani ya kikosi hicho kwani mpango wa muda mrefu wa Barcelona ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Xavi ambaye sasa anakinoa kikosi cha Al Sadd ya Qatar.

Author: Bruce Amani