Yuste Amtaka Messi Barcelona

Makamu wa Rais wa Barcelona Rafael Yuste amethibitisha kuwa wanaendelea na mazungumzo na matajiri Paris St-Germain kwa ajili ya kumrudisha mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Lionel Messi.

Messi, 35, aliondoka Barcelona mwaka 2021 na kujiunga na PSG akiwa ndiye kinara wa upachikaji klabuni hapo akifunga magoli 672 katika mechi 778.

Mkataba wa Messi na Paris St-Germain unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu ambapo matamanio ya mchezaji huyo ni kubakia kwa matajiri hao wa soka la Ufaransa.

“Leo na familia yake wanajua namna walivyo na thamani kwenye klabu yetu”, alisema Yuste.

“Messi anajua namna ambavyo tunathamini mchango wake hapa, tunaendelea kufanya mazungumzo kuona kama itatokea”, aliongeza.

Author: Asifiwe Mbembela