Mbappe Aipiku Rekodi ya Cavani PSG

Kylian Mbappe amekuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye Ligi Kuu nchini Ufaransa Ligue 1 kufuatia kufunga goli moja kwenye ushindi wa bao 3-1 walioupata Paris St-Germain dhidi ya Lens.

Ushindi huo unaifanya PSG kuwa kileleni kwa tofauti ya pointi tano ambapo sasa wanachuchumilia taji la Ligue 1 kwa mara ya 11.

Mbappe, alifunga bao la 139 kwenye mechi 169 akiipiku rekodi iliyokuwa inashikiliwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo na Manchester United Edinson Cavani.

Mabao mengine yakafungwa na Lionel Messi na Vitinha wakati bao moja la wabishi Lens likiwekwa wavuni na Przemyslaw Frankowski.

Hata hivyo, ushindi wa PSG ulikuwa mwepesi zaidi baada ya kiungo Salis Abdul Samed wa Lens kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 19 ya mchezo.

Author: Bruce Amani