PSG Yashinda Kwa Mbinde Mbele ya Lille

Paris St-Germain imefanikiwa kumaliza ukame wa ushindi kufuatia kuibuka na ushindi mgumu wa bao 4-3 dhidi ya Lille katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa Ligue 1 uliochezwa Parc Des Princess.

Katika mchezo huo, Paris walilazimika mara mbili kutokea nyuma na kurudisha kutoka kwenye mchezo wa namna yake, walianza wakiwa nyuma kwa bao 2-0 kabla ya kuwa 3-2 na mwishoni kushinda kibabe kwa goli la Lionel Messi dakika za lala salama.

Magoli ya Lille yamefungwa na Bafode Diakite, Jonathan David na Jonathan Bamba wakati yale ya wenyeji wa mtanange huo yakiwekwa kambani na Kylian Mbappe aliyeingia kambani mara mbili, Neymar Jr na mshindi wa Kombe la Dunia 2022, Messi.

Licha ya ushindi, PSG hofu kubwa itakuwa kuumia kwa fowadi wa timu ya taifa ya Brazil Neymar ambaye alitolewa nje kwa kubebwa kwenye machela, akiugulia maumivu.

Kwa matokeo hayo, PSG wanakaa kileleni mwa msimamo wa Ligue 1 kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya timu iliyonafasi ya pili Marseille.

Author: Bruce Amani