Lionel Messi atupia wakati Barcelona ikiichapa Mallorca 4-0

Barcelona imerudi vyema kufuatia ushindi wa goli 4-0 dhidi ya Mallorca mtanange uliopigwa Jumamosi hii ambapo mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi ameandikisha goli la 20 la msimu.

Alikuwa ni kiungo mkabaji Arturo Vidal ambaye alifunga mpira kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi wa Alba, kabla ya mshambuliaji Martin Braithwaite kuongeza goli la pili, Jordi Alba alipachika goli la tatu la Barcelona.

Baada ya kusaidia wengine kufunga, Messi alifunga goli la mwisho kwa Barca katika mchezo huo kwa shuti kali la mguu wa kulia, goli la 20 kwa msimu na assisti 14.

Wanacatalunya hao wanaongoza mbio za ubingwa kwa tofauti ya alama tano hivi sasa kabla ya Real Madrid haijacheza mchezo wake siku ya leo dhidi ya Elbar.

La Liga imerejea tena baada ya kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la virusi vya Corona huku taifa la Hispania likiwa miongoni mwa mataifa yaliyoathirika zaidi na Covid-19 ikiwemo Italia, Marekani, na China.

Author: Bruce Amani