Real Madrid waendelea kuyumba

Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wameshindwa kufunga bao katika michuano minne mfululizo, kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu mwaka wa 1985. Matatizo ya Los Blancos kushindwa kufunga bao sasa ndio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miongo mitatu baada ya kushindwa kutikisa wavu dhidi ya Deportivo Alaves.

Bao la Manu Garcia la dakika ya 95 liliwapa wenyeji Alaves ushindi wa kihistoria dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ulaya, na ambao unawaweka pointi sawa kwenye msimamo wa ligi na Real wakiwa na pointi 14 kila mmoja.

Real huenda wakajikuta katika nafasi ya nne kama viongozi wa ligi Barcelona, Sevilla na Atletico Madrid wote watashinda mechi zao za Jumapili.

Julen Lopetegui anasema anafahamu kuwa anakabiliwa na hali ngumu lakini kwa sasa hafikirii kuhusu kufutwa kazi. “makocha kila mara humulikwa, lakini hatuwazi kuhusu kuachishwa kazi,” Alisema Lopetegui katika kikao cha waandishi wa habari. “mambo hayaendi kama tulivyotaka. Tumesikitika bila shaka. Tulitaka kushinda. Tunajua namna maisha ya kocha yalivyo, na hasa katika Real Marid.” Alisema kocha huyo Mhispania.

Ameongeza kuwa bado ni mapema sana katika msimu na anataraji kuwa wachezaji wake ambao ni majeruhi watarudi hivi karibuni kwenye kikosi chake.

Author: Bruce Amani

AlavesReal madrid