Villarreal yatinga mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya

Villarreal imeibuka na ushindi wa goli 3-2 dhidi ya Atalanta katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mtanange wa mwisho uliopigwa Alhamis Disemba 9 baada ya awali mchezo huo kushindwa kuchezwa Jumatano kutokana na barafu kubwa kujaa uwanjani.

Wakati Villarreal chini ya kocha Unai Emery wakiingia kwenye mechi hiyo walikuwa wanahitaji alama moja ili kufuzu kucheza hatua ya 16 bora lakini wamevuna alama zote tatu wakiwa ugenini Bergamo.

Ushindi huo unaifanya Villarreal kuungana na Manchester United kutoka Kundi F kufuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa, wakishika nafasi ya pili.

Mabao ya Villarreal yamefungwa na Arnaut Danjuma aliyeingia kambani mara mbili na Etienne Capoue wakati yale ya Atalanta yamefungwa na Ruslan Malinovskyi na Duvan Zapata.

Droo ya 16 bora ya Uefa itafanyika Jumatatu Disemba 13 katika Jiji la Nyon, Switzerland.

Author: Bruce Amani