Juventus haitomtimua Pirlo licha ya hofu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Klabu ya Juventus imesisitiza kuwa haitamtimua kocha wake ambaye ni kiungo mshambuliaji wao wa zamani Andrea Pirlo licha ya hofu ya kupoteza nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2021/22.
Juventus ilikubali kichapo cha goli 3-0 kutoka kwa AC Milan Jana Jumapili na kuwaacha wakiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Italia – Serie A, ambapo mechi tatu zimesalia msimu kukamilika.
Pirlo alichaguliwa kuwa kurithi mikoba ya Maurizio Sarri mwishoni mwa msimu uliopita na chini ya utawala wake imetokea Juventus haijashinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangia mwaka 2012.
Baada ya matokeo mabovu kwenye mechi hiyo, Pirlo mwenye umri wa miaka 41 alisema “Sitabwaga manyanga”.
Kwa maana hiyo, Pirlo atakuwa kwenye kiti chake kwenye mchezo dhidi ya Sassuolo Jumatano, mechi dhidi ya Mabingwa Inter Milan na Bologna.
Juventus iko nyuma kwa tofauti ya alama moja kwa Napoli, alama mbili kwa Atalanta na AC Milan.

Author: Bruce Amani