Ibrahimovic Aweka Rekodi ya Serie A

Licha ya kikosi cha AC Milan kufungwa bao 3-1 dhidi ya Udinese, mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden Zlatan Ibrahimovic amefanikiwa kuandikisha rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao kwenye Ligi ya Serie A.

Ibrahimovic katika umri wa miaka 41 na. Siku 166 alifunga bao kwa mkwaju wa penati akimshinda mlinda mlango wa Udinese, Marco Silvestri bao ambalo linamfanya kuipiku rekodi ya Alessandro Costacurta ambaye alifunga bao akiwa na miaka 41 na siku 25.

Bao hilo ni muhimu kwa Zlatan ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeruhi.

Mabao ya Udinese yakafungwa na Roberto Pereyra, Beto na Kingsley Ehizibue akahitimisha utawala wa mchezo kwa Udinese kunako dakika ya 70.

Author: Asifiwe Mbembela