Barca yapata ushindi wa dakika ya mwisho dhidi ya Rayo

Barcelona imetanua uongozi wake kileleni mwa La Liga kwa pengo la pointi nne baada ya kutoka nyuma na kuishinda Rayo Vallecano 3-2 Jumamosi. Luis Suarez alifunga bao la ushindi katika dakika ya 90 baada ya Rayo kutoka bao moja nyuma. Mshambuliaji huyo wa Uruguay sasa ana mabao 9 katika La Liga msimu huu na ndiye anaongoza katika ufungaji magoli.

Lilikuwa bao lake la tano katika wiki moja na alipoulizwa kama anacheza vizuri bila ya Lionel Messi, kocha wa Barcelona Ernesto Valverde alijibu: “Nadhani wote wanacheza vyema na Messi.” Suarez alifungia Barca kabla ya Jose Pozo kuisawazishia Rayo, na Alvaro Garcia akawaweka kifua mbele katika kipindi cha pili. Nguvu mpya Ousmane Dembele alifunga la kusawazisha kabla ya Suarez kufunga la ushindi katika dakika ya 90

Ushindi huo uliiwezesha Barca kuitumia faida ya Atletico kushindwa kuilaza Leganes mapema Jumamosi. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 ambapo Guido Carillo alifunga bao la kuisawazishia Leganes baada ya Antoine Griezmann kuipa Atletico Madrid uongozi wa bao safi la free-kick

Awali, Real Madrid ilisonga hadi nafasi ya sita baada ya kushinda mchuano wao wa kwanza wa La Liga tangu Septemba  na kwa kiasi kikubwa kutokana na mchango wa kinda mwenye umri wa miaka 18 Vinicius Junior.

Waliwashinda Real Valladolid 2-0 lakini mechi hiyo haikuwa na bao kabla ya tineja huyo Mbrazil kuingizwa uwanjani dakika 17 kabla ya mchezo kuisha.

Shuti yake ya dakika ya 83 ilimgonga beki wa Valladolid Kiko Olivas na kuwapa Madrid bao la ufunguzi. Dakika tano baadaye akampa pasi Karim Benzema ambaye aliangushwa kwenye boksi. Sergio Ramos akafunga penalti na kumpa kocha wa mpito Santiago Solari ushindi wa mechi yake ya kwanza ya ligi. (DPA)

Author: Bruce Amani

BarcaRayo