Everton yamnyakua kinda wa Juventus Moise Kean

Everton imemsaini kinda wa Juventus mwenye umri wa miaka 19 anayechezea timu ya taifa ya Italia Moise Kean kwa mkataba wa miaka mitano. Kean alifunga mara nane katika mechi 21 akiwa Juve, klabu ambayo alijiunga nayo akiwa na umri wa miaka 10 na ameifungia Azzuri, (timu ya taifa ya Italia) mabao mawili katika mechi tatu.

Anakuwa mchezaji wa tano kuwasili Goodison Park katika kipindi hiki cha uhamisho wa msimu wa joto, kwa kitita ambacho hakikufichuliwa. Ila inakisiwa huenda kikawa pauni milioni 36. “Nnafuraha na fahari kubwa kuvaa jezi ya Everton. Nitajitolea kadri niwezavyo kuitumikia timu hii.” Alisema Kean.

Kocha wa Everton Marco Silva alisema “mshambuliaji alikuwa mmoja wa wachezaji wa kipaumbele kwetu msimu huu wa joto. Moise ana nguvu, kasi, na sifa nzuri za kuwa mshambuliaji na ana umri wa miaka 19 tu. ana kipaji na yuko tayari kufanya kazi, tayari kukiimarisha kikosi chetu na kutupa suluhisho tofauti.”

Kalbi hiyo tayari imemsaini kiungo wa Mainz Jean-Philippe Gbamin kwa mkataba wa miaka mitano wa kima cha pauni milioni 25.

Author: Bruce Amani