Ramsey asaini mkataba wa miaka minne na Juventus

Kiuno wa Arsenal Aaron Ramsey amesaini mkataba na miamba wa Italia Juventus, kwa ajili ya msimu ujao. Klabu hiyo imetangaza kuwa mchezaji huyo wa Wales atahamia Turin mwishoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka minne.

Juventus iliweka mtandaoni tangazo la kumsaini Ramsey

Ramsey anakamilisha miezi sita iliyobaki kwenye mkataba wake na The Gunners, ambao wamempa ruhusa ya kusaini makubaliano ya mapema na kuondoka Emirates mwishoni mwa msimu bila ada yoyote kutolewa. Juventus pia imesema italipa pauni milioni 3.7 kwa ajili ya usajili wa Ramsey.

Ramsey amewashukuru mashabiki wa Arsenal kupitia ujumbe wa Instagram, akiahidi kucheza kadri ya uwezo wake katika miezi iliyosalia kwa ajili ya kuisaidia timu yao.

“Mlinikaribisha nikiwa kijana mdogo na mmeniunga mkono katika nyakati nzuri na mbaya nilizopitia wakati nikiwa hapa. Nna huzuni moyoni kuwa naondoka baada ya miaka 11 ya kufana London Kaskazini.” Alisema Ramsey katika ujumbe wake. Arsenal pia ilitoa taarifa ikimshukuru mchezaji huyo wa Wales kwa wakati wake na katika timu hiyo tangu alipojiunga nao mwaka wa 2008 akitokea Cardiff City.

Author: Bruce Amani