‘Hatufikirii Ubingwa, Tunataka Kushinda Mechi Zetu” – Robert Matano

Tusker imeendelea kuvuna alama tatu kwenye mechi zake ambazo zimepelekea kuikaba koo Gor Mahia vinara wa Ligi Kuu nchini Kenya FKFPL ambayo imekuwa na mtihani katika kupata alama tatu kwenye mitanange inayoshiriki.

Ushindi mwembamba wa bao 1-0 walioupata Tusker FC mbele ya Police unaifanya timu hiyo kuwa alama moja pungufu ya vinara Mahia.

Kwenye mechi iliyochezwa uwanja wa Nyayo, nyuki walipata bao kupitia kwa Shaphan Siwa bao lililofungwa kipindi cha pili na kudumu kwa dakika 90.

Akizungumzia matokeo hayo, kocha wa Tusker Robert Matano amesema hawafikiri kuhusu ubingwa au kumkaribia kinara anachowaambia wachezaji wake wafikirie mechi ijayo dhidi ya Wazito.

Kocha wa Police ambaye ni kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Biashara United za Tanzania Francis Baraza amekiri kuwa hawakuwa bora vya kutosha kushinda huo mchezo.

“Tumefungwa kwa uzembe wetu kwa kweli, tumefanya makosa mengi sana kitu ambacho kilitokea hata kwenye mechi yetu na Gor Mahia”, alisema Baraza.

“Hatufikirii ubingwa, tunataka tuendelee kushinda mechi zetu kila wakati. Bado hatuja hesabu tofauti iliyopo ya pointi ila nawakumbusha wachezaji kwamba wafikirie mechi zetu”, alisema Matano ambaye msimu uliopita alishinda ubingwa dakika za jioni baada ya Kakamega Homeboyz kuongoza msimamo kwa muda mrefu.

Gor Mahia watakuwa na mechi Jumapili dhidi ya Posta Rangers wanaweza kuongeza pengo la pointi mbele ya nyuki, Tusker FC.

Author: Asifiwe Mbembela