Nahitaji kuzungumza na Messi, asema kocha mpya wa Barcelona Ronald Koeman

Kocha mpya wa Barcelona Ronald Koeman amesema hajui kama atamshawishi Lionel Messi kubakia klabuni hapo. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 57 amesaini mkataba wa miaka miwili na Barca, siku mbili baada ya klabu hiyo kumpia kalamu Quique Setien.

Mustkabali wa Messi katika dimba la Camp Nou haujulikani baada ya kushindwa kubeba Kombe msimu uliopita kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2007 – 08.

“Angali na mkataba na bado ni mchezaji wa Barcelona,” amesema Koeman. “Kwa wakati huu nahitaji kuzungumza naye kwa sababu ni nahodha.”

“Tunapaswa kufanya kazi naye na kuzungumza na wachezaji kadhaa. Tunapaswa kufanya maamuzi kadhaa lakini katika suala la Messi natumai atabaki nasi.

“Kama kocha, ningependa kufanya kazi na Messi kwa sababu anashinda mechi. Koeman alijiuzulu wadhifa wake wa kuifundisha timu ya taifa ya Uholanzi, huku akiwa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake.

Aliichezea Barcelona kati ya 1989 na 1995, na kuwasiadia kushinda mataji manne ya ligi na Kombe la Ulaya. Klabu hiyo imemtangaza Ramon Planes kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa kiufundi. Alikuwa naibu wa Eric Abidal, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake kama mkurugenzi wa spoti Jumanne.

Author: Bruce Amani