Nguli wa soka Misri afungwa mwaka mmoja

Mahakama moja nchini Misri imemhukumu Mohamed Aboutrika, mmoja wa wachezaji nguli wa soka katika historia ya taifa hilo, kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa makosa ya kukwepa kodi. Mahakama hiyo pia ilimpa Aboutrika mwenye umri wa miaka 40, chaguo la kulipa faini ya pauni za Misri 20,000, sawa na dola za Marekani 1,115 ili kusitisha adhabu yake katika uamuzi ambao unaweza kukatiwa rufaa. Aboutrika alihukumiwa bila kuwepo mahakamani.

Tangu alipostaafu soka amekuwa akiishi nchini Qatar ambako anafanya kazi kama mchambuzi wa soka. Misri ilizuwia mali za Aboutrika mwaka 2015 na kumuweka kwenye orodha ya watu wasioruhusiwa kusafiri kwa ndege mwaka 2017, kuhusiana na madai ya kuwa na mafungano na kundi la Udugu wa Kiislamu lililopigwa marufuku na kuorodheshwa kama kundi la kigaidi.

Author: Bruce Amani