Ole Gunnar Solskjaer arejea kuiokoa United, mara hii kama kocha

Ole Gunnar Solskjaer amepata jukumu jingine la kuiokoa Manchester United, mara hii kama kocha. Mshambuliaji huyo wa zamani ambaye alitambulika sana katika historia ya United kutokana na hasa alivyokuwa akifunga mabao muhimu na hasa akitokea benchi, ameteuliwa kuwa mtu atakayerejesha utulivu na kuliokoa jahazi la klabu hiyo ya England baada ya kipindi chamiaka miwili na nusu yenye misukosuko mingi chini ya Jose Mourinho. Solskjaer alifunga bao lililosalia kuwa maarufu sana miongoni mwa mashabiki wa United katika dakika za mejeruhi lililoipa United ushindi wa fainali ya Champions League 1999 dhidi ya Bayern Munich uwanjani Camp Nou.

Solskjaer amepewa mikoba ya ukocha hadi mwisho wa msimu, katika hatua inayolenga kurejesha tena imani ya mashabiki waliokuwa wamekata tamaa.

Jukumu lake: kupuliza tena pumzi katika United baada ya kuwa na mwanzo mbaya kabisa wa msimu wa ligi katika miaka 28. Timu hiyo inashikilia nafasi ya sita katika Ligi ya Premier, pointi 19 nyuma ya nambari moja Liverpool na 11 nyuma ya nambari nne Chelsea.

“Manchester United imo moyoni mwangu,” alisema Solskjaer mwenye umri wa miaka 45 ambaye aliichezea United kuanzia 1996-2007 na akafunga mabao 126 kati ya mechi 366, “na ni vizuri sana kuja tena hapa katika wadhifa huu. Nna hamu kubwa ya kuanza kufanya kazi na kikosi hiki chenye vipaji, wafanykazi na kila mmoja katika klabu.“ Solskjaer raia wa Norway amekuwa akiifundisha timu ya Norway ya Molde.

Author: Bruce Amani