Shabiki wa Chelsea akanusha kumrushia Sterling maneno ya kibaguzi

Shabiki mmoja wa Chelsea amekiri moja kwa moja kumrushia maneno ya kibaguzi winga wa Manchester City Raheem Sterling katika mechi iliyozikutanisha timu hizo katika dimba la Stamford Bridge ingawa amesema hakukusudia.

Uchunguzi uliofanywa na Polisi ya Uingereza uliomuonyesha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 akipigwa kelele na mashabiki wakati alipoenda kuokota mpira katika mtanange uliomalizika kwa Chelsea kuibuka na ushindi wa goli 2-0 uwanjani Stamford Bridge.

Mmoja wa mashabiki alietambulika alikiri kumtupia maneno Sterling ingawa anasema hayakuwa maneno ya kibaguzi hata kidogo.

“Najihisi kuwa mwenye aibu kutokana na tabia yangu na najisikia vibaya kweli, alisema Colin Wing, 60, akizungumza na gazeti la Daily Mail.

Wing aliongeza kwa kusema amekuwa akipendelea kulitumia neno Manc (mtu aliyekataa kwake au kwao-tafsiri isiyo rasmi) na sio neno black (mtu mwenye ngozi nyeusi) kwa kuwa anajua tofauti zake vizuri.

“Nimekuwa naingia uwanjani (Stamford bridge) kwa mwaka wa 50 sasa, na nnamulikwa na kamera kila mara. Hakika ningekuwa na tabia za kibaguzi ningekuwa nimekamatwa mda mrefu kwani kila siku huwa nakaa sehemu moja tu ya uwanja”. Aliongeza Mzee huyo.

Shabiki huyo amemwomba msamaha Raheem Sterling akisema amefukuzwa kazini kutokana na kitendo cha kibaguzi alichokionyesha katika mechi hiyo, pamoja na kunyang’anywa tiketi ya mwaka mzima.

Taarifa ya Chelsea inasema watu wanne wamekamatwa na kufungiwa kuingia uwanjani kwa mda wakati huo uchunguzi zaidi dhidi yao unaendelea, Chelsea imethibitisha itatoa ushirikiano kwa Polisi.

Author: Bruce Amani