Infantino apendekeza kuanzishwa ligi ya Afrika

Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema kuwa angependa kuona ligi ya Afrika ikiundwa na uwezekaji wa zaidi ya dola bilioni moja katika ujenzi wa viwanja barani humo. “Tunapaswa kuchukua vilabu 20 bora zaidi Afrika na kuviweka kwenye ligi ya Afrika,” Amesema Infantino wakati wa ziara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusherehekea miaka 80 ya kuzaliwa kwa klabu ya TP Mazembe.

“Ligi ya aina hiyo inaweza kutengeneza mapato ya karibu milionji 200, ambayo yanaweza kuiweka miongoni mwa 10 bora duniani,” aliongeza.

Infantino ameongeza kuwa anapanga kuzindua ombi la “kukusanya dola bilioni moja kabla ya kuweza kuipa kila nchi ya Kiafrika uwanja halisi wa kandanda unaofikia viwango vya FIFA.”

Infantino mwenye umri wa miaka 49 aliyechukua usukani kama rais wa FIFA mwaka wa 2016, amesema mawazo yake ni ya kuusaidia mchezo huo katika baraza la Afrika kushindana kwenye kiwango cha kimataifa. “Tutawachukua marefarii bora kabisa wa Afrika na kuwalipa. Tutaondoa siasa na kuweka utaalamu katika marefarii wa Afrika,” alisema.

Author: Bruce Amani