M-Bet Yaipa Simba Milioni 100 Kama Zawadi Kufika Robo Fainali CAFCL

Klabu ya Simba imevuna shilingi milioni 100,000,000 kutoka kwa Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo Kampuni ya Kubashiri ya M-Bet ikiwa ni makubaliano ya kutoa kiasi hicho cha fedha baada ya kufika hatua fulani ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hatua ya kutoa fedha hizo kwa kampuni ya M-Bet kunakuja kufuatia Wekundu wa Msimbazi Simba kuvuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali ya CAFCL wakipangiwa na Wydad Casablanca hatua hiyo.

Mkuruguenzi wa masoko wa Kampuni hiyo Allen Mushi amesema mwaka jana walisaini mkataba wa kutoa bonasi ya mafanikio fulani ambayo klabu itayapata na wataendelea kutoa fedha kila wanapofikia makubaliano hayo.

“Mwaka jana wakati tunasaini mkataba moja ya kipengele ni kutoa bonus kwa kila hatua wanayofika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuanzia hatua ya makundi. Leo tunatoa Tsh. 100 milioni na tunawambia tu kuna zingine zitakuja,” alisema Mushi.

Kwa upande wa Simba, Mtendaji Mkuu wa klabu Imani Kajula ameishukuru kampuni ya M-Bet kwa kuwapatia kifuta jasho ikiwa ni sehemu ya kutimiza makubaliano ya kimkataba.

“Tunawashukuru wadhamini wetu M-Bet kwa ushirikiano ambao wanatupatia. Leo watatukabidhi kishika mkono kwa kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” Kajula.

M-Bet wametoa fedha hizo kwenye kipindi ambacho Simba wametoka kushinda bao 2-0 dhidi ya Yanga lakini wakati wanaenda kucheza raundi ya kwanza ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad siku ya Jumamosi.

Author: Asifiwe Mbembela