Simba Yaifumua Yanga, Yasaka Ubingwa

Wekundu wa Msimbazi Simba wameibatua klabu ya Yanga bao 2-0 katika mchezo wa Kariakoo Derby ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mtanange uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Leo Jumapili.

Simba ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya nusu fainali mabao yake mawili yamefungwa kwenye kipindi cha kwanza, alianza Henock Inonga kufunga bao kunako dakika ya pili akimalizia kwa kichwa krosi ya Shomari Kapombe baada ya mpira wa kona.

Bao la pili likafungwa na Kibu Dennis dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kwa shuti kali baada ya mpira wa Khalid Aucho kupotea njia na kumkuta Kibu aliyekwamisha mpira nyavuni kwa shuti lililomshinda kipa Diarra.

Baada ya kipindi cha pili kuanza Yanga waliingia na uhai wa kusaka bao kwa kufanya mabadiliko matatu akitoka Abubakar Salum, Yannick Bangala na Jesus Moloko na nafasi zao kuchukuliwa na Mudathiri Yahya, Aziz Ki na Tuisila Kisinda.

Mabadiliko hayo yakaleta uhai kwenye kikosi hicho ingawa mpaka dakika 90 hakukuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya alama tatu kwenda kwa mnyama Simba ambaye bado anaendelea kushika nafasi ya pili kwa alama 63, mechi 26.

Simba wangekuwa na umakini kipindi cha kwanza wangeweza kufunga magoli zaidi kwani mara mbili Jean Baleke aligongesha miamba kutoka kwenye pasi za Clatous Chama.

Kipigo kinaifanya Yanga kusalia na alama 68 tano zaidi ya Simba baada ya zote kucheza mechi 26.

Author: Asifiwe Mbembela