Chelsea, Arsenal katika nafasi nzuri nusu fainali ya Europa League

Uwezekano wa kuwa na fainali ya Ligi ya Europa kati ya timu mbili za England unaendelea kuwa wazi baada ya Arsenal na Chelsea kujiweka katika hali nzuri katika mechi za nusu fainali Alhamisi usiku.

Arsenal itaelekea Uhispania kucheza na Valencia ikiwa kifua mbele mabao 3 – 1 baada ya kutoka nyuma kupitia mabao mawili ya mshambuliaji wa Ufaransa Alexandre Lacazatte na bao la dakika ya 90 la Pierre-Emerick Aubameyang katika dimba la Emirates.

Chelsea pia ilitoka nyuma na kupata sare muhimu ya 1 – 1 nyumbani kwa Eintracht Frankfurt nchini Ujerumani, huku Pedro akifunga bao muhimu la ugenini. Sare hiyo imeifanya Chelsea kuweka rekodi ya kuwa timu iliyocheza mechi nyingi za Europa bila kupoteza mechi yoyote kati ya 16.

Sio Arsenal wala Chelsea ambayo ina uhakika wa kumaliza katika nne bora kwenye Ligi ya Premier, ambayo hutoa tiketi ya moja kwa moja ya kufuzu Champions League msimu ujao. Kushinda Ligi ya Europa pia kunatoa zawadi hiyo, ndio maana timu zimeyachukulia mashindano hayo kwa umuhimu mkubwa

Fainali itachezwa mjini Baku, Azerbaijan mnamo Mei 29.

Author: Bruce Amani