Gor Mahia yakamata usukani wa ligi

Bao la dakika ya majeruhi kutoka kwa Mnyarwanda Jacques  Tuyisenge dhidi ya Bandari mjini Kisumu liliisaidia Gor Mahia kurejea kileleni mwa jedwali la KPL.

Bandari walionyesha mchezo mzuri katika kipindi cha kwanza na kubuni nafasi nyingi ambazo William Wadri, Yema Mwana na Abdallah Hassan walishindwa kutia kimyani.

Gor Mahia waliimarika kipindi cha pili na kuonyesha ari kubwa ya kuzoa alama tatu katika mchezo huo. Harun Shakava, Tuyisenge na Dennis Oliech wote walikuwa na nafasi za kufunga lakini walishindwa kumpiku kipa wa Bandari, Farouk Shikalo.

K’ogalo walizidisha mashambulizi na katika dakika ya majeruhi, walipata bao kupitia Nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda Tuyisenge ambaye alipiga tobwe la kichwa lililomzidi maarifa kipa wa Bandari.

Ushindi huo uliisaidia Gor kuchupa kileleni mwa jedwali kwa alama 49. Sofapaka ni wa pili kwa alama 48.

Gor itachuana na timu ya Mt. Kenya United siku ya Alhamisi nao Bandari watajibwaga uwanjani didhi ya AFC Leopards.

Author: Kevin Teya