Kampeni za kuwania nyadhifa za Yanga zaanza

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela ametangaza rasmi kuanza kwa kampeni za kuwania nafasi zilizowazi katika klabu ya Yanga baada ya mvutano wa TFF na Yanga ambapo sasa viongozi wa timu hiyo wamekubali kufanyika kwa uchaguzi Januari 13.

Akitangaza zoezi hilo Mwenyekiti huyo amewataka wagombea kufanya kampeni kwa amani bila kumchafua mwingine na mgombea anaruhusiwa kujinadi kokote ikiwemo katika tawi lolote la Young Africans ilimradi kuhakikisha anatunza amani.

Nafasi zinazogombewa ni pamoja na uwenyekiti ilioachwa wazi na Yusuph Manji, nafasi ya kaimu mwenyekiti Sanga, nafasi ya katibu ambayo pia iliachwa wazi na Charles Boniface Mkwasa.

Miongoni mwa wagombea walioanza kampeni zao ni Baraka Igangula mgombea wa nafasi ya uenyekiti ndani ya Yanga, ambaye amejinadi kulipa mishahara kwa wachezaji wote endapo atapewa ridhaa ya kuwa mwenyekiti kwa mda mfupi.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans ambaye pia ni Msaidizi wa Kaimu Mwenyekiti Siza Lyimo akiongea na Wanahabari amewataka Wanachama kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo ambao ana uhakika utakaokuwa wa amani na utulivu.

Uchaguzi wa Yanga unategemea kufanyika tarehe 13 Januari ambapo wananachama wa timu hiyo wamehimizwa kuhakiki kadi zao za Uwanachama mapema ili kupunguza usumbufu siku ya uchaguzi.

Author: Bruce Amani