Lyon yanyakua nafasi ya mwisho ya hatua ya mtoano

Mbili kati ya timu mbili kubwa za Ulaya zilijutia uamuzi wa kuvichezesha vikosi dhaifu katika usiku wa mwisho wa michuano ya hatua ya makundi ya Champions League.

Real Madrid ilipewa kipigo kibaya zaidi kuwahi kuikumba Ulaya nayo Manchester United ikishindwa kuchukua fursa ya kuongoza kundi lake. Katika usiku ambao Lyon ilisheherekea kuwa timu ya 16 na ya mwisho kutinga hatua ya mtoano, wachezaji wa Madrid walizomewa wakitoka uwanjani Santiago Bernabeu baada ya kukndamizwa mabao 3-0 dhidi ya CSKA Moscow. Ni kichapo chao kikubwa zaidi katika zaidi ya mechi 250 za nyumbani katika mashindano ya Ulaya.

Hata hivyo mabingwa hao watetezi walifuzu kama vinara wa kundi hilo.

Kama Madrid, United ilikiteuwa kikosi dhaifu hasa baada ya kujua tayari wamefuzu, hata ingawa timu hiyo ya Jose Mourinho bado ilikuwa na fursa ya kupanda juu ya Juventus katika nafasi ya kwanza kama ingeshinda.

Huku Juve yake Cristiano Ronaldo ikibumburushwa 2-1 dhidi ya Young Boys, United ingeibuka vinara lakini nao pia wakashindwa na matokeo sawa na hayo na Valencia.

Man Utd sasa itachuana na mmoja wa washindi wa makundi: Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Borussia Dortmund, Porto or Paris Saint-Germain. Utd ni moja ya timu za England zilizotinga hatua ya mtoano kwa msimu wa pili mfululizo.

Lyon yafuzu

Nafasi pekee ya kufuzu ilikuwa katika mchuano kati ya Lyon na Shakhtar Donetsk, na ni bao la Nabil Fekir la dakika ya 65 na kuipa Lyon sare ya 1-1 iliyohakikisha kuwa wanajiimarisha katika nafasi ya pili ya Kundi F nyuma ya Manchester City, ambayo iliizaba Hoffenheim 2-1. Shakhtar ilijiunga na Europa League. Bayern ilitoka sare ya 3-3 na Ajax Amsterdam. Sare hiyo iliipa Bayern fursa ya kuongoza Kundi E mbele ya Ajax. Timu zote zilikuwa tayari zimefuzu. Benfica tayari ilikuwa imejihakikishia nafasi ya tatu kabla ya kuipiku AEK Athens 1-0

Author: Bruce Amani