Maguire kuendelea kuwa nahodha wa Manchester United

Manchester United imethibitisha kuwa nahodha wao wa msimu uliopita Harry Maguire ataendelea kuwa kiongozi wa timu hiyo katika msimu mpya ambao unaanza leo Jumamosi.

Akizungumzia kuelekea kuanza kwa msimu mpya kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema Maguire ambaye ni raia wa England ataendelea kuwa kepteni wa timu hiyo kwa 2020/21.

Maguire, 27, alikumbwa na kazia ya kutoa maneno yasiyo mazuri kwa Jeshi la Polisi la Ugiriki na kujaribu kutoa rushwa alikokuwa kwenye mapumziko binafsi baada ya timu yake kutolewa nje ya michuano ya Europa Ligi na Sevilla ya Hispania.

Bado kesi yake inaendelea kuunguruma kule Ugiriki juu ya makosa ya mchezaji huyo wa zamani wa Leicester City ambapo yeye(Maguire) mara zote amekuwa akikana madai hayo.

“Ataendelea kuwa kepteni wetu”, alisema Solskjaer. “Amekuwa akikiongoza kikosi chetu vizuri, hakika nitaendelea kuwa nyuma yake katika hili”.

Maguire amemwachia Mwanasheria wake kila kitu katika kushughulika ishu hiyo lakini bado hadi sasa hakuna uwazi zaidi ya tukio hilo.

Awali nahodha huyo wa United alijitoa kwenye kikosi cha England ambacho kilikuwa kinajiandaa kumenyana vikali kwenye mechi mbili za Ligi ya Mataifa lakini kuna uwezekano akarudishwa mwezi Octoba na kocha Gareth Southgate.

United watacheza dhidi Aston Villa mchezo wa kirafiki siku ya leo Jumamosi wakijiandaa na kabumbu ambayo itaaanza Sept 19 dhidi ya Crystal Palace dimbani Old Trafford kwa upande wao.

Author: Bruce Amani