Manchester United yakomaa zaidi kwa Jadon Sancho wa Borussia Dortmund

Manchester United wamefikia pazuri katika kukamilisha uhamisho wa winga wa timu ya taifa ya England na Borrusia Dortmund Jadon Sancho. Mashetani Wekundu hao, ni kama wameamua kuvunja kibubu cha kukubali mshahara wa mchezaji huyo na ada ya wakala huyo kwa lengo la kukamilisha usajili wa “mtu anayetajwa kuwa tegemeo la usajili dirisha hili kubwa”

Licha ya hatua hizo, lakini bado hakuna makubaliano yoyote ambayo yamefikiwa baina ya Borussia Dortmund na Manchester United ambapo Dortmund wanahitaji pauni milioni 120 wakati United wanaonekana wakiwa na kinyongo na pesa hiyo kuelekea mwishoni mwa dirisha la usajili Octoba 5.

Baadhi ya ripoti zinadai kuwa huenda Dortmund wakashusha bei ya staa huyo endapo dirisha la usajili litakaribia kufungwa bila kujitokeza kwa timu zenye uwezo wa kumnunua, ingawa pia pauni milioni 100 zinaweza kukubaliwa.

Wiki iliyopita Manchester United walikamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uholanzi na Ajax Donny van de Beek kwa dau la pauni milioni 35 na kuwa usajili wa kwanza kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Sancho, 20, amekuwa akihusishwa kujiunga na timu mbalimbali barani Ulaya kutokana na ubora aliokuwa nao kwenye msimu wa 2019/20, timu kama Real Madrid, Barcelona, Paris Saint Germain na Manchester United ni miongoni mwa klabu zenye nia ya kumsaini winga huyo raia wa England.

Author: Asifiwe Mbembela