Simba ipo kamili kuivaa Ruvu Shooting, Mkude na Shiboub kukosekana

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara Simba SC wanashuka dimbani leo Jumapili katika dimba la Taifa kumenyana na Ruvu Shooting majira ya saa kumi jioni ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa timu hizo baada ya ligi kusimama kwa takribani miezi mitatu kwa sababu ya Covid-19.

Kuelekea mchezo huo wenye kuvuta hisia ya namna yake kwa wanachama na mashabiki wa soka Tanzania, Simba ambayo utakuwa mchezo wa 29 itawakosa mastaa wake wawili Jonas Mkude (majeruhi), na Sharaaf Shiboub (yuko Sudan bado).

Ukiachana na hao wawili, wachezaji wake wote wapo fiti, Miraj Athuman, ‘Sheva’ alikuwa nje kwa muda mrefu akitibu majeraha hivyo kutumika kwake leo licha ya kuwa yupo fiti kutategemea maamuzi ya mwalimu.

Clatous Chama, kiungo wa Simba, huyu alichelewa kuanza mazoezi na wenzake kwa kuwa Zambia mipaka ilikuwa imefungwa pia hivyo naye ni maamuzi ya mwalimu iwapo ataona anafaa kuvaana na Ruvu Shooting.

Hadi hivi sasa, Simba anaongoza msimamo wa ligi kuu kwa tofauti ya alama 25 kwa timu iliyonafasi ya pili na tatu. Katika mechi ya Jumamosi, Yanga walipata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Mwadui FC

Author: Bruce Amani