Simba yataka uwanja wake, mchango wapitishwa

Ile kauli inayosema kuwa upatapo shida ndipo ujulikanapo mlango wa kutokea, basi usemi huu unasadifu vyema kunako viunga vya Msimbazi Kariakoo baada ya klabu ya Simba kupitia Murtaza Mangungu ambaye ni Mwenyekiti wa klabu hiyo kusema wanahitaji michango ya takribani bilioni 30 kujenga uwanja wao.

Simba wamefikia hatua ya kujenga uwanja wao kupitia michango ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo baada ya Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Barbara Gonzalez kufanyiwa ukilitimba wakati akijaribu kuingia uwanjani kutazama mtanange wa Simba na Yanga uliopangwa wikiendi iliyopita na kumalizika kwa sare tasa.

Huenda walikuwa na wazo hilo kweli, lakini ukilitimba ule kwa Barbara pamoja na waandamizi wengine wa Simba umeongeza mzuka zaidi, saizi ni michango tu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Ijumaa Disemba 17, 2021 wakati wa uzinduzi wa kampeni za kuchangia Uwanja huo, Mangungu amesema ni jambo zuri kuwa na Uwanja wao.

“Jambo hili sio geni kwa kuchanga kwa sababu hata slogani yetu ni Simba nguvu moja, makadirio ya Uwanja huu ni takribani Bilioni 30,” amesema Mangungu.

Mangungu amesema Rais wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ameshaanza kwa kuchangia Sh2 bilioni na pesa hizo sio sehemu ya uwekezaji wake.

Naye Mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema anashukuru kwa Rais wa klabu hiyo Mohammed Dewji kuchangia ujenzi wa Uwanja .

“Tumepigiwa simu nyingi sana na leo tumeamua kuzindua rasmi kampeni zetu kuhusu Uwanja huu, tunajua Simba wana nia ya kuchangia uwanja wao,” amesema Barbara.

Barbara amesema ;” Kwasasa kamati imekaa na bodi kwa ajili ya michoro ya ramani, mwezi wa kwanza michoro rasmi itatoka.”

Uwanja wa Simba unatarajia kuingiza watu sio chini ya elfu thelathini (30000).

Wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba wanachangia kupitia mitandao ya simu pamoja na benki.

Author: Asifiwe Mbembela