Simba yatoa somo kwa wanafunzi wa Alliance

Mabingwa watetezi wa kandanda ya ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019, Simba SC wameibuka na ushindi wa goli 4-1 dhidi ya Alliance Football Club katika mtanange wa vuta ni kuvute uliopigwa dimba la CCM Kirumba leo Jumapili.

Ikiwa katika ziara ya Kanda ya Ziwa Simba imefanikiwa kujikusanyia alama sita kibindoni kufuatia kuibuka na ushindi kwenye mechi mbili, ule wa Mbao 2-1 na huu wa sasa.

Wekundu wa Msimbazi hao walianza kuandikisha ushindi kupitia kwa Jonas Mkude aliyekuwa anasawazisha goli la mapema la Israel Mwenda upande wa Alliance, kisha kipenga cha mwamuzi Martini Sanya kikakamilisha ungwe ya kwanza matokeo yakiwa 1-1.

Ungwe ya pili ilikuwa imeegemea zaidi upande wa Simba ambapo ilifunga goli tatu ndani ya dakika chache kupitia kwa Meddie Kagere, Clatous Chama na Hassan Dilunga walihusika katika goli za leo kila mmoja akiwa amefunga goli moja.

Goli la Meddie Kagere “MK 14” linakuwa na 11 msimu huu akiwa amehusika katika jumla ya goli 15 baada ya kusaidia goli 4 msimu huu.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 41 wakati Alliance Fc wakiwa na pointi 20 nafasi ya 13.

Author: Bruce Amani