TFF yawatakatisha Mukoko Tonombe na Cedric Kaze wa Yanga

Kiungo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Mukoko Tonombe, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Oktoba kwa msimu wa 2020/21 huku Cedric Kaze pia wa timu hiyo akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Mukoko na Kaze walitwaa tuzo hizo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mwezi huo wa Oktoba, Yanga ilicheza michezo minne, ikiwa ndiyo timu iliyoshinda michezo yake yote na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 18. Yanga ilizifunga Coastal Union 3-0, Polisi Tanzania 1-0, KMC 1-2 na  Biashara United, 0-1 ambapo Mukoko alitoa mchango mkubwa katika ushindi huo ikiwa ni pamoja na kufunga bao moja dhidi ya Polisi Tanzania.
Mukoko  aliwashinda mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube na  mshambuliaji wa Gwambina FC, Meshack Abraham aliongia nao fainali, ambapo Dube aliiongoza Azam kubaki kileleni baada ya kuvuna pointi 10 katika mwezi huo, ikishinda tatu, sare moja na kupoteza moja, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao matatu na kutoa pasi tatu za usaidizi wa mabao.
Kwa upande wa Meshack aliiongoza Gwambina  kupata pointi nane ikishinda michezo miwili, sare miwili na kupoteza mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 14 akiifungia timu yake mabao manne.
Kwa upande wa Kaze aliwashinda Aristica Cioaba wa Azam na Francis Baraza wa Biashara United ambapo Kaze aliiongoza Yanga katika michezo mitatu na kushinda yote. Yanga chini ya Kaze ilizifunga Polisi Tanzania, KMC  na Biashara United na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.
Cioaba aliiongoza Azam  kushinda michezo mitatu, sare moja na kupoteza moja, huku Baraza akiiongoza Biashara kushinda michezo mitatu na kupoteza miwili ikipanda kutoka nafasi ya saba hadi ya nne.

Author: Bruce Amani