Winga wa Yanga Morrison ajikuta kizuizini baada ya kutofautiana na polisi barabarani

Winga wa klabu ya Yanga Bernard Morrison ameingia katika skendo nyingine ya kukamatwa na Jeshi la Polisi la Kinondoni baada ya kutofautiana kauli akiwa kwenye gari lake leo Alhamis Julai 30.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Rodgers Bukombe amesema Morrison alikamatwa baada ya kuwa mkaidi kufuatia gari lake kutiliwa shaka na Polisi lakini alipohitajika kusimamisha alionyesha ukaidi kidogo.
“Askari walihisi harufu ya kitu kutoka ndani ya gari yake, sasa walipotaka kumfanyia upekuzi akagomea upekuzi huku akileta utata akitaka kuwarekodi polisi, baadae Polisi walifanikiwa kumtaka waelekee kituo cha polisi kwa hatua zaidi akakubali na akatoa maelezo yake pale kituo cha Polisi Oysterbay.
Utakumbuka mwanzoni mwa mwezi wa 7 ziliibuka taarifa kuwa winga huyo wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini aliwashikia kisu walinzi waliokuwa wakimzuia asitoroke kambini akiwa na kikosi cha Yanga SC jijini Dar es Salaam pamoja na utovu wa nidhamu mwingine ambao umekuwa ukitajwa mara kadhaa.
Hata hivyo, Winga huyo raia wa Ghana ambaye amekuwa akikumbwa na matukio mengi nje ya uwanja aliachiliwa huru muda mfupi baada ya kupelekwa kituo cha Polisi.

Author: Asifiwe Mbembela