Azam yawaalika Wagosi wa Kaya Coastal Union VPL

Klabu ya Azam Fc inashuka dimbani leo kumenyana vikali dhidi ya Coastal Union katika dimba la Azam Complex majira ya saa moja kamili usiku leo Ijumaa ukiwa ni mtanange wa raundi ya pili baada ya pazia la Ligi Kuu nchini kufunguliwa wiki iliyopita. Azam iliyochini ya kocha Aristica Cioaba ilianza mchezo uliopita kwa ushindi mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mtanange uliopigwa dimba pia la Azam Complex ambapo strika Obrey Chirwa ndiye aliyefunga bao pekee katika ushindi huo.

Wakati huo huo, Wanakuchele wanaonolewa na Juma Mgunda walikutana na kichapo cha goli 1-0 dhidi ya mwanafainali wa Kombe la FA Namungo Fc kwenye mechi iliyopigwa Lindi.
Katika siku za karibuni Azam wamekutana mara nne na Coastal Union mara nne ambapo mechi 2 zimeenda kwa Wanakuchele na moja imeenda kwa Wanarambaramba na sare moja, ambapo mchezo wa mwisho uliisha kwa Coastal Union kuisha na goli 2-1 mtanange uliopigwa dimba la Azam Complex mwezi Februari.
Ratiba ya michezo mingine ya VPL itaendelea mwishoni mwa wiki hii ambapo Simba, Yanga na timu nyingine zitakuwa katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ambao hivi sasa unashikiliwa na Simba Sports Club.

Author: Asifiwe Mbembela