Moto wa Simba hauzimiki, yaitafuna Coastal Union

Mabingwa watetezi wa TPL Simba wamefanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga na kupindua meza kwa kutoka nyuma kwa goli moja.

Simba ilitanguliwa kufungwa mapema kabisa kunako dakika ya kwanza kupitia makosa ya Erasto Nyoni na Aishi Manula, makosa hayo yakatumiwa vyema na Razini Hafidh

Bao hilo lilidumu mpaka kipindi cha pili ambapo Simba walianza kuwanyanyua mashabiki dakika ya 49 kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Coastal Union kumchezea rafu Emanuel Okwi ndani ya 18 iliyozamishwa kimiani na Meddie Kagere.

Licha ya uwanja kutokuwa rafiki kutokana na hali ya uwanja na uwepo wa jua kali uwanjani kutokana na mchezo kufanyika mapema, kikosi cha Simba kilionyesha kandanda safi  mpaka dakika ya 68 ambapo Meddie Kagere alipofunga goli la pili kupitia pasi mpenyezo ya Mzambia Clatous Chota Chama. Goli lililowapa Simba alama tatu Mkwakwani, jijini Tanga.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 60 baada ya kucheza michezo 23 huku wakisalia kwenye nafasi yao ya tatu kwani kinara ni Yanga mwenye pointi 74 ambaye amecheza michezo 32.

Kwa msimu huu ni mara ya kwanza Simba kupindua matokeo kwani mchezo wa kwanza kupoteza walianza kufungwa na Mbao FC msimu uliopita dakika ya 16 na Said Junior bao lililodumu mpaka dakika ya 90 Uwanja wa CCM Kirumba.

Katika michezo 23 Simba imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Mbao FC.

Author: Asifiwe Mbembela