Simba amtafuna Yanga katika mtanange wa watani wa jadi

Simba imeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Kariakoo Derby wa Ligi Kuu Tanzania bara uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi ya 16 ukiwa ukiwa ni mtanange wa mkondo wa pili msimu huu.

Katika mchezo huo Simba walionekana wakiutawala kwa asilimia kubwa baada ya kutengeneza nafasi za wazi kupitia kwa Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Bocco lakini hazikutumiwa vizuri.

Kipindi cha pili kilianza kwa kocha Patrick Aussems alifanya mabadiliko ya kumtoa Clotous Chama na kumuingiza Hassan Dilunga ambaye aliongeza ufanisi katika eneo la kiungo.

Dakika ya 77 ya kipindi cha pili juhudi binafsi kutoka kwa Nahodha wa klabu ya Simba John Bocco ziliweza kuisaidia timu hiyo kupata goli pekee katika mchezo huo kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga kwa kichwa na kumuacha kinda Ramadhan Kabwili asijue la kufanya.

Baada ya goli hilo Kocha Mwinyi Zahera alifanya mabadiliko kadhaa ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda pale alipomtoa Amisi Tambwe, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu na nafasi zao kuchukuliwa na Mrisho Ngassa, Matheo Simon na Mohammed Issa.

Matokeo hayo yanaendelea bado kuibakiza Yanga kileleni mwa msimamo wa TPL ikiwa na alama 58 katika michezo 24 tofauti na Simba walio nafasi ya 3 alama 39 katika michezo 16 ambayo imecheza mpaka sasa.

Huu ulikuwa mchezo wa pili kwa walimu wote wawili Patrick Ausseums na Mwinyi Zahera, ingawa Patrick anaonekana kufanya vizuri katika michezo hiyo baada ya kushinda moja na sare moja huku Zahera anaweza akajitetea kutokana na ufinyu wa kikosi chake.

Mbio za ubingwa kwa pande zote mbili ziko wazi ambapo Simba ikishinda viporo vyake vilivyobakia itaweza kukwea mpaka nafasi ya kwanza bila kuangalia matokeo ya timu nyingine.

Author: Asifiwe Mbembela