Yanga tayari kufanya Biashara katika mtanange wa FA

Klabu ya Yanga inaingia dimbani kesho Alhamisi kumenyana na Biashara FC kutoka Mara mchezo wa raundi ya 4 wa Kombe la Shirikisho la TFF utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, saa moja jioni.

Kuelekea mchezo huo Yanga imeweka bayana wachezaji watakaokosekana kutokana na majeraha ambao ni Jaffary Mohammed na Baruani Akilimali huku kikosi hicho kikipata nguvu mpya baada yakurejea kwa Raphael Daud “Rotti” na Juma Mahadhi.

Akizungumza na Waandishi wa habari katika Makao ya timu hiyo Kariakoo kuelekea mchezo huo Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amesema “Kesho tunacheza na Biashara ya Mara FA ambapo mchezo utafanyika saa moja usiku, viingilio vya mchezo vitakuwa 10,000 na 3,000″, Alisema Ten.

Kombe la TFF lipo katika mkondo wa nne, ambapo huchezwa kwa mtoano endapo Yanga itaibuka na ushindi hapo kesho Alhamisi, itakutana na Namungo FC ya Lindi inayoshiriki ligi daraja la kwanza katika muendelezo wa kusaka nafasi ya uwakilishi wa nchi kwa upande CAF.

Biashara FC inaingia katika mtanange huo ikiwa na kumbukizi ya kupoteza dhidi ya Azam FC mchezo wa ligi, ingawa tangu Amri Said ” Stamp” aingie kunako timu hiyo akitokea Mbao Fc imekuwa katika kiwango bora tofauti na mzunguko wa kwanza.

Yanga nayo imepoteza michezo yake miwili mfululizo mmoja wa ligi dhidi ya Stand United na mwingine wa mashindano ya Sportpesa Supercup dhidi ya Kariobangi Sharks. Huu utakuwa ni mchezo wa pili ndani ya msimu mmoja baada ya ule wa kwanza Biashara kuangukia pua kwa kukubali kichapo cha goli 2-1 mchezo uliofanyika Uwanja wa taifa pia.

Author: Bruce Amani