Bayern Yachechemea Chini ya Tuchel, Dortmund Wavutwa Nyuma

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya nchini Ujerumani Bundesliga Bayern Munich wameendelea kuchechemea kwenye Ligi hiyo kufuatia sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Hoffenheim mchezo uliochezwa uwanja wa Allianz Arena

Bayern ambayo ipo chini ya kocha Thomas Tuchel imeshinda mechi mbili kati ya tano ambapo kwa sare hiyo, sasa wanaongoza msimamo wa Bundesliga kwa tofauti ya pointi mbili kufuatia matokeo ya sare ya 3 – 3 ya Borussia Dortmund mbele ya Stuttgart.

Akizungumza baada ya mchezo, Tuchel ameonyesha kutokubaliana na wachezaji kwa namna ambavyo wamecheza kwani walishindwa kuonyesha matamanio ya kufanya vizuri kulinganisha na namna walivyofungwa na Manchester City Jumanne iliyopita.

“Leo tumeshindwa kuonyesha njaa ya kushinda, tulikuwa tunacheza kawaida wakati tulipaswa kuonyesha hasira zaidi ya mechi iliyopita (City)”.

Benjamin Pavard alifunga bao la uongozi kwa Bayern kabla ya Andrej Kramaric kusawazisha kwa mpira wa kutengwa.

Kwingineko, Dortmund wametoa sare ya 3-3 na Stuttgart wakati RB Leipzig imeichapa 3-2 Augsburg.

Author: Bruce Amani