Bayern Yaichapa 4-2 Dortmund

Thomas Tuchel ameanza vyema kwenye utawala wake Bayern Munich kufuatia kuiongoza timu hiyo kuinyuka Borussia Dortmund bao 4-2 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ujerumani Bundesliga, mtanange uliopigwa dimba la Allianz Arena Jumamosi.

Mabao ya Bayern ambayo kabla ya mchezo huo walikuwa wanashika nafasi ya pili yamefungwa na Dayot Upamecano, Thomas Muller aliyefunga mabao mawili na Kingsley Coman.

Wakati upande wa Dortmund ambayo imekuwa na msimu mzuri yamefungwa na Emre Can kwa penati kisha Donyell Malen akaongeza bao la pili ambalo halikusaidia kubadilisha chochote kwenye magoti ya Bayern.

Licha ya ushindi huo kuonekana ni mkubwa, bado Bayern walikuwa na uwezo wa kufunga mabao zaidi kwani magoli ya Eric Maxim Choupo-Moting na Serge Gnabry yalikataliwa.

Matokeo hayo yanaifanya Bayern kukwea mpaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Ujerumani Bundesliga wakiwa juu ya Borussia Dortmund kwa tofauti ya pointi mbili.

Author: Bruce Amani