“Hatutavumilia Uvunjifu wa Amani” – Tuchel

Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel amesema hawawezi kuvumilia vitendo visivyo na maadili kwa mchezaji yeyote klabuni hapo.

Tuchel amesema hayo wakati akizungumzia tukio analotuhumiwa nalo Sadio Mane kuwa alimpiga Kofi midomoni winga wa Kijerumani Leroy Sane baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City uliomalizika kwa Bayern kufungwa bao 3-0 Etihad.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal amesimamishwa kutoshiriki mchezo wa Ligi ya Bundesliga dhidi ya Hoffenheim Jumamosi kutokana na kitendo hicho ambapo pia inaelezwa kuwa atatakiwa kulipa faini.

“Kila mmoja ana haki ya kufanya makosa. Nafahamu Sadio vizuri ni mchezaji ambaye hazingatii mambo mengi nje ya uwanja mara nyingi anafanya kila unalomweleza, namwamini sana”, alisema kocha Tuchel ambaye alionyesha imani kwa Mane mshambuliaji wa zamani wa Southampton na Liverpool za England.

“Hata kama amesimamishwa bado anatakiwa kuwepo mazoezini, najua atapewa faini pia”.

Ripoti zinaeleza sababu ya Mane kumpiga Sane ni baada ya kutolewa kauli za kuudhi na winga huyo wa zamani wa Manchester City baada ya mchezo wa Uefa na City.

Author: Bruce Amani