Brazil, Hispania zafuzu nusu fainali ya Olimpiki Tokyo 2020

Timu ya Taifa ya Brazil imeibuka na ushindi mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya Misri katika mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Olimpiki Tokyo 2020 mtanange uliopigwa Jumamosi Julai 31 Japan.

Bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na Matheus Cunha lilidumu kwa dakika zote tisini na kufanikiwa kutimba hatua ya nusu fainali, wakibakiza ushindi kwenye mechi mbili ili kuvishwa ushindi wa medali.

Brazil watachuana vikali na Mexico Jumanne hatua ya nusu fainali ya kwanza wakati nusu fainali nyingine itakuwa baina ya Japan dhidi ya Hispania.

Wenyeji Japan walishinda kwa penati 4-2 baada ya dakika kumalizika kwa sare tasa, Hispania ikitokea nyuma imeshinda bao 5-2 dhidi ya Ivory Coast kwenye muda wa ziada na Mexico wameshinda bao 6-3 dhidi ya Korea Kusini.

Author: Asifiwe Mbembela