Brazil yafuzu fainali ya Olimpiki Tokyo 2020, wenyeji Japan watupwa nje

Timu ya taifa ya wanaume ya Brazil imefuzu kucheza hatua ya fainali ya Olimpiki Tokyo 2020 baada ya kuifunga Mexico kwa mikwaju ya penati kufuatia sare tasa katika dakika 120.

Brazil ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, wameshinda mikwaju ya penati kwa 4-1, katika mchezo uliopigwa Kashima huko Japan.

Mlinda mlango wa Brazil Santos aliokoa mkwaju wa Eduardo Aguirre kabla ya tuta la Johan Vasquez kugonga mtambaa wa panya ikiwa ni penati ya pili.

Watamenyana vikali dhidi ya timu ya taifa ya Hispania siku ya Jumamosi Agosti 7, 2021 baada ya timu hiyo kuitoa Japan.

Waliofunga penati kwa Brazil ni Dani Alves, beki Gabriel Martinelli, Bruno Guimaraes na Reinier.

KWINGINEKO, kiungo mshambuliaji wa Real Madrid Marco Asensio alikwamisha mpira nyavuni kunako dakika za lala salama ya 115 na kuipa nafasi Hispania kufuzu hatua ya fainali.

Ni fainali ya kwanza kwa Hispania kufuzu hatua hiyo ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2000.

Author: Asifiwe Mbembela