Cedric Kaze wa Burundi atajwa kuwa Kocha mpya wa Yanga kumrithi Luc Eymael

Yanga imemtaja atakayekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo kwa msimu ujao baada ya kuwa bila kocha kufuatia kutimuliwa kwa Luc Eymael mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019/20.

Wakizindua “Wiki ya Wananchi” katika Makao makuu ya nchi Jijini Dodoma Yanga kupitia kwa Mwenyekiti wa timu hiyo yenye masikani yake Twiga na Jangwani Jijini Dar es Salaam imesema Kocha mpya tayari wamempata Cedric Kaze ambaye ni raia wa Burundi na atatua klabuni muda wowote baada ya kukamilika kwa taratibu za usafiri.
Akizungumzia kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Yanga, Dkt Mshindo Msola amesema “Mnaouliza kuhusu Kocha, tumeshampata Cedric Kaze kutoka nchini Burundi ambaye alikuwa Canada na taratibu zinaendelea za ujio wake nchini tayari kuanza kazi ya kuinoa timu yetu”.
Yanga ilikuwa haina Kocha tangu luc Aymael kutimuliwa baada ya mchezo wa mwisho kwenye ratiba ya msimu uliopita kufuatia kutoa maneno yaliyo tafsiriwa kuwa ya kibaguzi kwa mashabiki na wadau na soka nchini Tanzania.
Inakuwa mara ya tatu mfululizo kwa Timu ya Wananchi kuwatumia Waalimu 3 kwenye misimu mitatu tofauti baada ya kuanza na Mwinyi  Zahera ambaye alidumu kwa msimu mmoja na nusu, Luc Eymael ambaye ni sawa amekaa klabuni hapo kwa msimu mmoja na sasa wamempa timu Mburundi.
Kocha Kaze ana uzoefu mkubwa kwani ameinoa timu ya daraja la juu Burundi ya Mukura SC na anaweza kuungana na kocha wa zamani wa makipa wa Azam Fc ambaye amewai kufanya nae kazi Vildamiri Niyonkuru

Author: Asifiwe Mbembela